Nuru FM

DC aagiza wazazi 191 wakamatwe

13 November 2022, 11:22 am

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Jamhuri William ameagiza kukamatwa kwa wazazi wa wanafunzi 191 ambao hawajafanya mtihani wa kidato cha pili kutokana na utoro, ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Msako huo wa nyumba kwa nyumba utaenda sambamba na kuwakamata wanafunzi watoro na kuwarudisha shuleni, huku mkuu huyo wa wilaya akieleza baadhi ya wazazi ndio chanzo cha wanafunzi kutohudhuria shuleni kutokana na kuwatumia kwenye shughuli za kiuchumi.

Akizungumza kwenye baraza la madiwani la halmashauri hiyo, William alisema Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya elimu bure, hivyo kitendo cha wanafunzi 191 kushindwa kufanya mtihani ni kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha kila mwanafunzi anafanikiwa kupata elimu msingi ambayo ni darasa la kwanza hadi kidato cha nne.


Pia aliagiza kufanyika tathmini ya utoro kwenye madarasa ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ili kubaini ukubwa wa tatizo na kuja na njia ya nini kifanyike kumaliza tatizo hilo.

Ofisa elimu sekondari wa halmashauri hiyo, Patrick Atanas alisema mimba za utotoni, mwamko mdogo wa wazazi kuhusu elimu, shughuli za migodi, ufugaji na kilimo ni miongoni mwa sababu za wanafunzi hao wa kidato cha pili kutofanya mtihani wa Taifa.

Alisema halmashauri hiyo yenye shule 12 za sekondari, wanafunzi 2,157 wa kidato cha pili waliandikishwa kufanya mtihani wa Taifa ulioanza Oktoba 31, hadi Novemba 11, 2022, lakini wakati mitihani hiyo ikiendelea wanafunzi 191 wamebainika kutoingia kwenye vyumba vya mtihani.

“Wapo wazazi wanawalazimisha watoto wafeli, ili wasiendelee na shule. Upande mwingine wanafunzi wana shida wenyewe hawapendi kusoma, sisi kama idara ya elimu tunachofanya ni kuwaelimisha waone umuhimu wa elimu wawekeze kwenye masomo,” alisema .