Nuru FM

Mbunge Kabati Awataka wananchi wasiwafiche walemavu siku ya sensa

11 July 2022, 8:48 am

Wananchi Mkoani Iringa wametakiwa kuacha kuwaficha watu wenye ulemavu katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika hapa nchini tarehe 23/8/2022.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Iringa  Mh. Ritta Kabati ambaye Pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Ritta Kabati Trust Fund wakati wa kongamano la watu wenye ulemavu lililoasisiwa na Taasisi yake katika viwanja vya Garden Posta Mkoani hapa.

 

Mh. Kabati amesema kuwa watu wenye ulamavu wana wajibu wa kushiriki katika zoezi la sensa kwa kuwa litaisaidia serikali kupata takwimu sahihi za watu hao ambazo zitasaidia kupata Fursa mbalimbali zilizopo katika serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia suluhu Hassan ikiwemo Mikopo, Fursa za elimu, ujasiriamali, Kijamii na kisiasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika kongamano hilo la watu wenye ulemavu amesema kuwa kundi hilo lina wajibu wa kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi huku akiwataka wazazi wenye watoto au familia yenye watu wenye ulemavu kutokuwaficha katika zoezi hilo.

 

Awali akizungumzia kuhusu Umuhimu wa sensa ya watu na Makazi Mratibu wa zoezi hilo na Mtakwimu wa Halmshauri ya manispaa ya iringa Raymond Nyanzwa amesema kuwa takwimu muhimu za watu wenye ulemavu zitaisaidia serikali kujua ni idadi kiasi gani ya kundi hilo inahitaji kutatuliwa changamoto zao.

 

Kwa upande wake Mjumbe wa halmashauri Kuu CCM Taifa Theresia Mtewele amesema kuwa Chama cha Mapinduzi CCM kimejipanga kuhakikisha kinatoa elimu kupitia viongozi wao kuanzia ngazi ya Mtaa hadi kitaifa ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki katika zoezi la sensa ya mwaka huu ambayo ni ya sita toka Tanzania iungane na Zanzibar mwaka 1964.

 

Zoezi La Sensa Husadia Serikali Kupata Taarifa Za Msingi Zitakazosaidia Mchakato Wa Utekelezaji Wa Dira Ya Maendeleo Ya Mwaka 2025, Mageuzi Ya Masuala Ya Afya Na Jamii, Pamoja Na Ufuatiliaji Wa Ajenda Za Maendeleo Za Kimataifa