Nuru FM

Soko kuu Iringa kufanya kazi mpaka saa nne usiku

14 March 2024, 10:48 am

Wafanyabiashara wa soko Iringa mjini wakiendelea na majukumu yao. Picha na Ayoub Emanuel

Kitendo cha wafanyabiashara wa soko kuu la Iringa mjini kuruhusiwa kufanya biashara zao mpaka saa nne usiku kimeonekana kuwa msaada kwa wananchi wanaotaka huduma hizo.

Na Azory Orema

Licha ya soko kuu Manispaa ya Iringa kuruhusiwa kufanya biashara mpaka saa 4 usiku wafanyabiashara katika eneo hilo wameomba serikali iongeze miundombinu ya ulinzi ili kuboresaha upatikanaji wa huduma bora kwa wateja wao.

Akizungumnza na Nuru Fm moja kati ya wafanyabiashara wa soko kuu hilo Philip Kembe amesema kwa sasa kumekuwa na mwamko mdogo huku akitarajia kuongezeka siku za usoni.

Kwa upande wake mwenyekiti wa soko kuu Manispaa ya Iringa ndugu Rafael Ngulo amesema mtazamo wao ni kuhakikisha soko hilo linatoa huduma masaa 24 kama miji mingine.

Sanjari na hilo Mwenyekiti huyo amesema ulinzi na usalama katika eneo hilo umeimarishwa hivyo wananchi wanatakiwa kwenda kupata huduma bila shaka yoyote.

Soko kuu la Manispaa ya Iringa na soko la Mlandege yaliyopo mkoani hapa ndio masoko pekee yaliyopewa nafasi ya kufungwa saa 4 usiku kutokana na mahitaji ya wafanyabiashara na wateja ikiwa ni kilio cha muda mrefu.