Nuru FM

Madiwani Iringa, ASAS watoa msaada kwa wanafunzi wenye uhitaji

22 May 2023, 8:33 pm

Baadhi ya madiwani Manispaa ya Iringa wakikabidhi msaada wa mahitaji kwa wanafunzi. Picha na Mwandishi wetu.

Na Mwandishi wetu

Madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa kushirikiana na kampuni ya ASAS DAIRIES wametoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya msingi Katumba II iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Madiwani wamekabidhi zawadi kadhaa ikiwemo fedha zaidi ya shilingi laki 2 kama motisha kwa walimu na wanafunzi, mifuko ya sukari na mchele, vinywaji na mafuta ya kupikia huku kiwanda cha ASAS kikitoa kiasi cha lita 50 za maziwa bure kwa ajili ya kuboresha lishe ya wanafunzi.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni kukamilisha ziara ya mafunzo ya madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Iringa iliyoanza Mei 19, 2023 kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya ya Rungwe.

Awali madiwani walipata fursa ya kutembelea katika shamba la mkulima katika kijiji cha Kalalo ambapo walijifunza kilimo cha tija ambapo mkulima hujishughulisha na ufugaji.

Ndugu Juma Mwakifulefule ni mfugaji aliyetembelewa ameeleza kuwa shamba lake lina ekari 7 kila mwezi anavuna mikungu 100 na kupata kiasi cha shilingi milioni 2 na kila mkungu huuzwa kwa wastani wa shilingi 20,000/=

Aidha amesema samadi ya ng’ombe hutumika kurutubisha shamba la migomba na kwa idadi ya mifugo yake huzalisha lita 200 kwa siku sawa na wastani wa pato la shilingi 140,000/= kwa siku.

Pia walitembelea kiwanda cha gesi (TAL GAS) wamejifunza namna gesi inavyozalishwa na kuuzwa katika viwanda vya kusindika vinywaji ndani na nje ya nchi.

Gesi hii husambazwa katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro na nchi za Zambia, Kenya na Zimbabwe.

Ibrahim Ngwada ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa anasema ziara hiyo ina maana kubwa sana kwa wajumbe wa baraza la madiwani kwani wamejifunza mambo mengi mazuri ambapo wataenda kuyafayia kazi na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Halmashauri.