Nuru FM

Mafinga Mji wagawa vifaa vya usafi

24 June 2023, 9:38 am

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Regnant Kivinge akizungumza baada ya kukabidhi Vifaa vya usafi. Picha na Sima Bingileki

Na Sima Bingileki

Halmashauri ya Mji Mafinga imekabidhi vifaa 11 vya kutunzia taka kwa uongozi wa Stendi Kuu ya mabasi Mafinga na Stendi ya Matanana lengo likiwa ni Kuimarisha Usafi wa Mazingira na uhifadhi mzuri wa taka hasa katika maeneo ya mikusanyiko ya watu.

Akizungumza mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Mafinga Mheshimiwa Regnant Kivinge amesema kuwa lengo la halmashauri ya Mji Mafinga ni kuona wananchi wanaishi katika mazingira mazuri na taka zinatunzwa sehemu sahihi bila kuleta madhara kwa wananchi kama mlipuko wa magonjwa.

Amesema vifaa hivi vya kutunzia taka ni mazao ya ushindi iliyopata halmashauri ya Mji Mafinga mwaka 2022 kitaifa kwa kushika nafasi ya pili Usafi wa Mazingira na kufanikiwa kupata zawadi shilingi milioni 10.

Moja ya Kifaa Cha kuhifadhia Taka kilichotolewa na Halmashauri.

Fedha hizo zimetumika kuweka uzio kwenye makaburi ya Meti na kutengeneza vifaa vya kuhifadhia taka 11 ambavyo 7 vitawekwa stendi kuu ya mabasi na 4 vitawekwa stendi ya matanana.

“ kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, tusitupe taka hovyo kwani usafi ni tabia tuhakikishe mji wetu ni msafi na taka tuziweke kwenye vifaa vyake, Halmashauri inaandaa sheria ndogo ya kutupa taka hovyo hivyo tujiandae kuisimamia lengo ni kushika nafasi ya kwanza usafi wa mazingira kitaifa na kuwawezesha wananchi kuishi mazingira safi na bora”

Akizungumza mmoja wa wananchi mfanyabiashara katika eneo la stendi kuu ndugu Makombe Nasa amesema kuwa hakika watakuwa mabalozi wazuri wa kutunza usafi katika eneo la stendi na vifaa hivyo vitasaidia sana kuiweka stendi katika hali ya usafi kwani mwanzo havikuwepo hivyo wameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa kujali usafi wa eneo hilo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na waheshimiwa Madiwani, wataalamu wa Halmashauri, viongozi wa stendi kuu ya mabasi mafinga na wananchi wa Halmashauri ya mji mafinga na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa taka na usafi wa Mazingira Ndugu Charles Tuyi ambaye alihudhuria kama Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga.