Nuru FM

Simba SC yatangaza mpango wa ASFC

20 May 2022, 7:13 am

Uongozi wa Simba SC umetangaza rasmi kuweka kambi jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaowakutanisha dhidi ya Young Africans Jumamosi (Mei 28), katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Simba SC imetangaza rasmi mpango huo, baada ya kikosi chao kuondoka jijini Dar es salaam jana Alhamis (Mei 10) majira ya jioni kuelekea jijini Mwanza, tayari kwa mchezo wa Mzunguukozo wa 25 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold, siku ya Jumapili (Mei 22).

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema baada ya mchezo dhidi ya Geita Gold FC, kikosi chao kitaendelea kusalia Mwanza, kwa maandalizi ya kuikabili Young Africans Jumamosi (Mei 28).

Amesema Uongozi wa Simba SC umeamua kufanya hivyo kutokana na mchezo wa Nusu Fainali ya ASFC kupangwa kuchezwa jijini Mwanza, na wao tayari wameshatua jijini humo, hivyo wamedhamiria kutumia wasaa huo ili kufikia lengo la kujiandaa vizuri na hatimaye waibuke kidedea.

“Mbali na kujipanga kuweka kmabi Mwanza, hili ni lengo letu la pili naomba ieleweke hivyo, kilichotuleta Mwanza kwa sasa ni mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold, baada ya hapo tutaingia kwenye mkakati wa kuikabili Young Africans.”

“Michezo hii miwili ina umuhimu mkubwa sana kwetu, dhidi ya Geita ni kwa sababu ya kutengeza hali ya kujiamini kwa wachezaji wetu kuelekea Nusu Fainali ya ‘ASFC’, mchezo dhidi ya Geita pia utakua ni kwa sababu ya kurudisha tabasamu kwa Wanasimba kuelekea mchezo wetu wa Nusu Fainali ya ‘ASFC’.” amesema Ahmed Ally

Wakati Simba SC wakijipanga kuanza kambi ya kujiandaa na Nusu Fainali ya ASFC baada ya kuikabili Geita Gold FC Jumapili (Mei 22), Young Africans nao wana mpango wa kwenda Mwanza kuweka kambi baada ya mchezo wao dhidi ya Mbeya Kwanza FC utakaopigwa leo Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.