Nuru FM

RC Dendego aagiza wanafunzi wapokelewe bila kikwazo

8 January 2024, 2:22 pm

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego akizungumzia kuhusu Elimu na walivyoanza kuwapokea wanafunzi.

Na Joyce Buganda
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amewaagiza Walimu na Wakuu wa Shule wote Mkoani humo kuwapokea bila vikwazo wanafunzi wote wanaojiunga na kidato cha kwanza na wale wanaoanza elimu ya msingi.

Ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kutembelea shule za msingi na sekondari zilizopo katika manispaa ya Iringa mapokezi na mahudhurio ya wanafunzi hao ambapo akiwa katika shule ya sekondari kwavava iliyopo kata ya kitwiru Mhe. Dendego amesema kuwa kutokana na familia kutofautiana kiuchumi viongozi wa shule wawapokee Watoto hao hata kama hawana sare wapokelewe na kuanza kusoma na mambo mengine yatatekelezwa mwanafunzi akiwa darasani anasoma.

Dendego ameongeza kwa kusema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Sare anachokitazama ni akili ya wananfunzi hivyo amewaomba wazazi na walezi ambao bado hawajawapeleka Watoto wao shuleni kwa visingizio vya kukosa sare za shule basi kwa sasa wawapeleke shuleni Watoto wao.

Pia Dendego amewaasa wananfunzi hao kuzingatia masomo wawapo shuleni na kwa upande wa wasichana wasikubali kurubuniwa na kujiingiza katika vishawishi vitakavyopelekea kuacha masomo na kupoteza ndoto zao.

Kwa upande wa wavulana Mhe. Dendego amesema “niwatake wanafunzi wa kiume msome kwa bidii na kuacha kwenda kwenye vijiwe vya mitaani muache kukimbilia maisha kwani kila kitu kina muda wake wakati huu ni wakusoma kwanza”

Nae mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Veronika Kessy ametoa shukrani nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwaajili ya ujenzi wa shule hizo jambo ambalo limeondoa adha ya wanafunzi Kwenda umbali mrefu kupata elimu

Akitoa taarifa ya shule ya sekondari kwavava mkuu wa shule hiyo Mwalimu Vicky Katanga amesema wamepokea wanafunzi 140 ambapo wanafunzi ambao wameanza kushirikiana nao ni wanafunzi 98 na mpaka sasa wamepokea wanafunzi 63, nae Mwalimu mkuu wa shule ya msingi kitwiru Mwalimu Salome Sanga amesema mpaka sasa wameandiskisha wanafunzi 104

Nao baadhi ya wazazi wameishukuru serikali kwa kuwajengea shule ya sekondari Kwavava wakisema kuwa awali wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu Kwenda shuleni lakini kwa sasa watakuwa karibu na shule hiyo na pia mahusiano kati ya mwalimu mzazi na mwanafunzi yatakuwa mazuri.

Kwa upande wao wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari wameishukuru serikali na kuahidi kuwa kwa nafasi waliyoipata watahakikisha wanasoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao.