Nuru FM

Serikali Kufanikisha Kujenga Vyuo Vya Veta Kwa Kila Wilaya Nchini

4 July 2022, 3:52 pm

Serikali imefanikiwa kujenga vyuo kadhaa ambapo kuna vyuo takribani 43 vya VETA ambavyo vinafanya kazi lakini pia kuna vyuo 39 ambavyo vinajengwa na ifikapo mwezi Julai mwishoni kutakuwa na Vyuo takribani 78 vya VETA nchini.

Ameyasema hayo leo Julai 4,2022 Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde mara baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Amesema adhima ya Serikali ni kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na Chuo cha VETA ili vijana kuanzia shule ya msingi mpaka elimu ya juu anapomaliza masomo lazima awe na ujuzi fulani.

“Serikali inataka sasa kijana anapomaliza masomo yake iwe darasa la saba au la sita akitoka pale aweze kujitegemea kwa njia moja ama nyingine “. Amesema Dkt.Mbonde.

Aidha amesema katika mwaka huu wa Fedha, Serikali imetoa Bilioni 100 ili vijengwe Vyuo vingine 36 vya Wilaya hivyo kufikia zaidi ya Vyuo 100 ifikapo mwisho wa mwaka ujao hapa nchini

Pamoja na hayo ameshauri vijana wa Kitanzania kujaribu kuona umuhimu wa kujiunga na vyuo vya VETA ili angalau tusiangaike mitaani kwani ukifika VETA hutokosa kujifunza ujuzi wa aina yoyote unayoipenda.

“Nawaomba vijana wakitanzania mvitumie vizuri vyuo hivi ili muweze kupata ujuzi na muweze kufanya kazi kwa maendeleo ya Taifa letu kuliko kukaa tu na kuzurura mitaani”. Amesema

Nae Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za vijana ambao wamekuwa wakifanya ubunifu kwa kuhakikisha huduma zitokanazo na ubunifu zinatumika katika taasisi za Serikali pamoja na kwenye sekta binafsi.

Hata hivyo ameipongeza VETA kwa kuendelea kukuza bunifu kutoka kwa wabunifu ambao wamekuwa wakijiunga na Chuo hicho kwaajili ya kukuza bunifu zao na kuweza kusaidia vijana wengi kujiajiri na hata wengine kuajiriwa kwa urahisi kutokana na ubunifu wao.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Bw.Anthony Kasore amesema ujuzi  ambao wanawapatia vijana na wananchi kwa ujumla ni lazima wahakikishe pia unaendana sambamba na mahitaji ya soko la ajira nchini.