Nuru FM

TBS yatoa wito kwa wazalishaji na waingizaji wa mabati nchini kuzingatia viwango

13 October 2022, 5:32 am

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji na waingizaji wa mabati nchini kuhakikisha wanazingatia viwango ili kuzalisha mabati bora.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Usimamizi wa Sheria TBS, Bw.Moses Mbambe amesema bidhaa za mabati ambayo yanaingia  nchini wamekuwa wakiyakagua kwa kuchukua sampuli na kupeleka  maabara ili kujiridhisha na ubora wa viwango vya bidhaa hiyo.

Amesema wakibaini bidhaa hiyo haijakidhi viwango huchukua jukumu la kumtaka  mwenye bidhaa arudishe bidhaa ilipotoka  ama aiteketeze kwa kutumia  gharama za mwenye bidhaa.

“Mwenye bidhaa anajukumu la kuiteketeza bidhaa yake ikiwa tumebaini  haijakidhi viwango vya ubora, na kama tukijiridhisha inakidhi  viwango basi, tunampatia cheti cha ubora na kumruhusu bidhaa zake kuingia sokoni”. Amesema

Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Usimamizi wa Sheria TBS, Bw.Moses Mbambe akizungumza na waandishi wa habari

Aidha amesema shirika la viwango huwa wanafanya ukaguzi katika soko kuhakikisha mabati yanayouzwa hapa nchini yanakidhi vigezo vya ubora kwa mujibu wa viwango husika, wanakwenda katika maghala ya waingizaji wa mabati pamoja na maduka yanayouza mabati kuchukua sampuli kwaajili ya kwenda kupima na wakibaini hayajakidhi viwango huchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake Afisa Viwango TBS, Mhandisi Arnold Mato amesema matakwa ya viwango vya ubora wa bidhaa za mabati ni vipimo kama unene , urefu na upana ikiwa ni pamoja na migongo .

“Katika vipimo vya unene mara nyingi tunaangalia unene ambao unaanzia geji 30-32, 28,26, lakini bidhaa zote hizi mwisho ni geji 30  na kama  kuna atakayezalisha geji zaidi ya 30 mfano 32 basi takwa la kiwango linamtaka mzalishaji huyo kuandika ili kumjulisha mteja kwamba bati hilo sio kwa matumizi ya kuhezekea”.

Afisa Viwango TBS, Bw. Arnold Mato akizungumza na waandishi wa habari