Wananchi Ulanda waomba kukarabatiwa barabara
23 July 2026, 10:30

Wananchi wa Kata ya Ulanda wamesema kuwa barabara inayounganisha Kata ya Ulanda na maeneo jirani haijaimarishwa kwa kujengwa makaravati.
Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga, Wilaya ya Iringa, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara za vijiji vya kata hiyo, wakisema hali ya barabara imeendelea kuwa kero kubwa, hususan kipindi cha mvua.
Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, wananchi wa vijiji vya Mwambao, Weru, Lupalama na Kibebe walisema kuwa, licha ya utekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo, barabara inayounganisha Kata ya Ulanda na maeneo jirani bado haijaboreshwa kwa kujengwa makaravati, jambo linalosababisha magari kushindwa kupita wakati wa mvua.
Aidha, wananchi hao walimuomba Mbunge wao kueleza ni lini barabara hizo zitafanyiwa matengenezo, wakisema walipatiwa ahadi hiyo tangu mwaka 2019 lakini hadi sasa haijatekelezwa. Walisema hali hiyo pia imekuwa ikiwasababishia wanafunzi kupata shida kufika shuleni, hasa kipindi cha mvua.

Akijibu changamoto hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, alisema jimbo hilo hupokea takribani shilingi bilioni 3.5 kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya zaidi ya kilometa 900 za barabara.
Hata hivyo, alisema fedha hizo hazitoshelezi kutekeleza mahitaji yote yaliyopo, hivyo Serikali hulazimika kuweka kipaumbele kwenye barabara zilizoharibika zaidi na zisizopitika kabisa.
Kiswaga alifafanua kuwa Serikali imeiomba mamlaka husika kufanya tathmini upya ya mtandao wa barabara ili kuongeza fedha za matengenezo na kuboresha huduma hiyo.
Alisema mkakati wa muda mrefu ni kubadilisha barabara nyingi za udongo kuwa za changarawe ili kupunguza gharama za matengenezo na kuongeza uimara wake kwa muda mrefu.
