Tanroad Iringa yaanza kuboresha Daraja la Ipogolo
19 August 2026, 10:53

Maboresho haya katika eneo la Ipogolo ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara ya Ipogolo – Kilolo.
Na Hafidh Ally
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Iringa tayari umeanza utekelezaji wa Maboresho katika Daraja la Ipogolo lililopo kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa ili kuimarisha mkondo wa maji uliopita kwenye Barabara hiyo Kuu ya TANZAM sambamba na kujenga karavati la kuzuia athari za mafuriko wakati wa msimu wa mvua.
Akizungumza katika eneo la Ipogolo baada ya kufunga barabara hiyo Afisa Ustawi wa Jamii TANROADS Mkoa wa Iringa Alex Mgongolwa amesema wamechukua hatua hiyo ili kuziwahi mvua ambazo zinatabiriwa kunyesha na mamlaka ya hali ya hewa.
Aidha Mgongolwa amesema kuwa Tanroad imezingitia masuala ya usalama kwa kuweka vibao vya kuongoza magari wakati wa ujenzi ili kukamilisha kazi kwa wakati.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Mhandisi Mwanaisha Rajab anasema ujenzi wa karavati hili ni sehemu ya mradi wa Barabara ya Ipogolo hadi Kilolo inayojengwa kwa zaidi ya bilioni sitini za Kitanzania.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa wamesema kuwa kuboreshwa kwa daraja hilo itasaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu wakati wa mvua huku wengine wakisema njia hiyo kufungwa imeongeza mzunguko wa safari.
Maboresho haya katika eneo la Ipogolo ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara ya Ipogolo – Kilolo yenye urefu wa kilomita 33.61 kwa kiwango cha lami, mradi unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 60.
