Nuru FM

Serikali yaombwa kuongeza Watumishi na Wodi Ihongole

25 August 2026, 10:30

Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, akizungumza na wananchi. Picha na Fredrick Siwale

Uhaba wa watumishi katika Kituo cha afya ihongole unahatarisha usalama wa wagonjwa wanaofika kituoni hapo kupata huduma za afya.

Na Fredrick Siwale

Wananchi wa Kata ya Boma, Halmashauri ya Mji Mafinga, wameiomba Serikali kuongeza watumishi wa afya pamoja na wodi katika Kituo cha Afya Ihongole, ili kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Wananchi hao wameyasema hayo wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, ambapo wameeleza kuwa uhaba wa watumishi wa afya unasababisha baadhi ya wagonjwa kuchelewa kupata huduma na wakati mwingine kupoteza maisha.

Sauti ya Wananchi

Aidha, wananchi hao wamesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya, huku wakiomba pia ufafanuzi kuhusu gharama halisi za kadi za kliniki kwa mama wajawazito.

Sauti ya Wananchi
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Daktari Matilda Daud Yassin akitolea ufafanuzi maswali ya wananchi.

Akizungumzia changamoto hizo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Daktari Matilda Daud Yassin, amesema Halmashauri hiyo imefanikiwa kupokea watumishi wa afya 78, ambao tayari wamepelekwa katika Kituo cha Afya Ihongole.

Sauti ya Kaimu Mganga

Aidha, Daktari Matilda amekiri kuwepo kwa uhaba wa wodi za watoto, wanawake na wanaume katika kituo hicho, huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya, ikiwemo kukipatia kituo hicho friji la kuhifadhia maiti pamoja na mashine ya X-ray.

Sauti ya Matilda

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, amesema Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kadri bajeti zinavyopatikana, huku akisisitiza umuhimu wa kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye mahitaji makubwa.