Kiswaga atoa mabati 55 kukamilisha ujenzi wa darasa Mlandege
4 July 2026, 09:40

Mabati hayo ni nyongeza ya mchango alioutoa awali katika mradi huo baada ya tathmini kubaini kuwa yaliyokuwepo hayakutosha kukamilisha ujenzi wa darasa hilo.
Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga, ameendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuboresha sekta ya elimu baada ya kutoa mabati 55 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa darasa katika Kijiji cha Mlandege, Kata ya Mseke.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo wakati wa ziara yake ya kikazi jimboni, Mhe. Kiswaga alisema lengo ni kuhakikisha darasa hilo linakamilika kwa wakati ili wanafunzi wapate mazingira bora na salama ya kujifunzia.
Katika mkutano huo, aliwashukuru wananchi wa Kalenga kwa ushirikiano na imani wanayoendelea kumuonesha, akieleza kuwa ziara yake inalenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kutoa mrejesho wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kueleza vipaumbele vya Serikali kufuatia kuhitimishwa kwa kikao cha Bajeti ya Serikali bungeni.
Mbunge huyo alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ili kuboresha maisha ya wananchi.
Alieleza kuwa kati ya vitongoji 455 vya Jimbo la Kalenga, vitongoji 331 tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme, huku Serikali ikiendelea na jitihada za kufikisha huduma hiyo katika vitongoji vilivyosalia ndani ya kipindi kilichopangwa.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Mhe. Kiswaga alisema Serikali inaendelea kutafuta njia za kuimarisha mpango wa ruzuku ya mbolea na kupanua masoko ya mazao ya wakulima ili kuongeza tija na kipato.
Pia aliwahamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza gharama za matibabu.

Awali, Diwani wa Kata ya Mseke, Alex Kadinda, alimpongeza Mbunge huyo kwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwa kuitikia mahitaji ya wananchi kwa vitendo.
Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha changamoto mbalimbali, zikiwemo ukosefu wa zahanati, huduma ya maji safi na salama, umeme katika baadhi ya vitongoji, ujenzi wa kalavati, kuanzishwa kwa stendi ya mabasi Mlandege, pamoja na kushuka kwa bei ya mazao ya kilimo.
Akijibu hoja hizo, Mhe. Kiswaga aliahidi kuendelea kuzifuatilia kwa kushirikiana na Serikali, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa sauti ya wananchi wa Kalenga bungeni na kushirikiana nao kuhakikisha maendeleo ya jimbo hilo yanaendelea kupatikana.