Nuru FM
Nuru FM
12 May 2026, 09:09

Ajali hiyo imehusisha basi la abiria la kampuni ya THE CLASSIC linalofanya safari kati ya Zimbabwe na Tanzania pamoja na lori la mizigo, ambapo magari hayo yaligongana uso kwa uso.
Na Hafidh Ally
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, kutembelea na kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya barabarani iliyotokea alfajiri katika Kijiji cha Uyole, Kata ya Mseke, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Akizungumza hospitalini hapo, Mhe. Kheri amewapa pole majeruhi wa ajali hiyo na kuwahakikishia kuwa wataendelea kupata huduma vizuri na afya zao zitarejea kama hapo awali.
Aidha, Mhe. Kheri amewapongeza madaktari na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa juhudi na moyo wa kujitoa katika utoaji wa huduma kwa Wagonjwa

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Alfred Mwakalebela, amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu wawili pamoja na majeruhi 13, ambapo amesema kuwa kati ya majeruhi hao, watu 8 ni raia wa Zimbabwe na 4 ni raia wa Zambia.
Baadhi ya abiria ambao wamenusurika ktk ajali hiyo wameelezea kile ambacho wamekiona huku wengi wakisema tukio hilo limewakuta wangali wakiwa usingizini.
Ajali hii imetokea ikiwa ni siku chache tangu kushuhudia ajali nyingine iliyohusisha basi la abiria la kampuni ya SHABBIBY na lori aina ya Howo lililokuwa limebeba shehena ya soda aina ya Pepsi katika Kijiji cha Tanangozi, Kata ya Mseke, iliyosababisha vifo vya watu watano na wengine kujeruhiwa.