Nuru FM
Nuru FM
4 May 2026, 07:43

“Pasipokuwa na amani, hata malengo binafsi ya mtu mmoja mmoja ya Mtanzania mmoja mmoja hayawezi kufikiwa,”
Na Hafidh Ally
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini ili kuimarisha maadili, mshikamano wa kijamii na kudumisha amani ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Dkt. Nchemba amesema hayo aliposhiriki ibada katika kanisa kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mufindi, lililopo Mafinga Mjini, mkoani Iringa na kuongeza kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema, inayozingatia misingi ya haki na uwajibikaji.
“Serikali inaendelea kusisitiza Watanzania wote kuwa wadau wa kuombea na kusimamia amani ya nchi yetu,” amesema.

Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mufindi, Dkt. Anthony Kipangula, ameipongeza serikali kwa kazi ya kuwahudumia wananchi na kusisitiza kuwa ziara za Waziri Mkuu zimeonesha uongozi unaowagusa wananchi moja kwa moja.
“Nimeona juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwajali wananchi mtu wa ngazi yako kushuka mpaka kusikiliza kesi ya mwananchi na kumruhusu ajieleze, niliona ni maajabu kabisa,” amesema.
Hata hivyo serikali kupitia Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchema amepongeza juhudi za Kanisa katika malezi ya watoto na vijana na kuongeza kuwa mafanikio ya mipango ya maendeleo ya Taifa yanategemea uwepo wa amani.
