Milioni 402 zatolewa kwa vikundi 28 Iringa
2 July 2026, 11:13

Serikali imeendelea kusisitiza uwezeshaji wa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na kuimarisha uchumi wa kaya.
Na Hafidh Ally
Jumla ya vikundi 28 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Manispaa ya Iringa vimekabidhiwa mikopo yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 402.26 kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Akitoka taarifa ya Utekelezaji wa mpango wa Serikali wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Iringa, Mwatum Dossi amesema Katika mgawanyo huo, vikundi vya wanawake vimepatiwa shilingi milioni 152.5,Vikundi vya vijana vimekabidhiwa shilingi milioni 153.36, na Kwa upande wa watu wenye ulemavu, wamepokea shilingi milioni 96.4.
Ameeleza kuwa miongoni mwa vigezo hivyo ni kuwa na mradi unaoonekana na wenye tija, kuwa na nyaraka halali za usajili na biashara pamoja na mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za kifedha.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kupitia fedha za marejesho ya mikopo pamoja na asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Alisema katika bajeti ya mwaka huo, halmashauri ilitenga Sh milioni 793.67 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu awamu ya kwanza, lakini kutokana na marejesho mazuri ya mikopo ya awali, kiasi kilichotolewa hadi kufikia Machi 2026 kilifikia Sh milioni 799.99, kikinufaisha vikundi 69 vyenye wanachama 330, wakiwemo wanaume 67 na wanawake 263.
Akihitimisha hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewataka wanufaika kuiona mikopo hiyo kama mtaji wa maendeleo na si fedha za matumizi ya kawaida kwani serikali ina dhamira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.
Licha ya Manispaa ya Iringa kutokuwa na mapato makubwa ikilinganishwa na baadhi ya halmashauri nchini, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi agizo la Serikali la kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya makundi maalumu.