Nuru FM
Nuru FM
9 May 2026, 09:36

Viongozi hao wametakiwa kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia maadili, haki, usawa, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kutekeleza masuala ya umma
Na Hafidh ALLY
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka Wakuu wa Taaaisi na Viongozi Mkoani humo kuheshimu utawala wa sheria na kuzingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa semina maalumu iliyowakutanisha wakuu wa taasisi na viongozi waandamizi wa Mkoa wa Iringa, Mhe. James amesema Semina ni muhimu katika kuimarisha dhana ya utawala bora pamoja na uwajibikaji serikalini.
Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swela, amesema lengo la semina hiyo ni kuwakumbusha viongozi hao wajibu wao wa kuzingatia maadili, uadilifu na uwazi katika utendaji kazi wao ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Leonard Daudi Kanisimba, amesema kupitia semina hiyo wamewakumbusha viongozi umuhimu wa kuzingatia maadili ya uongozi na kuepuka vitendo vinavyokiuka misingi ya utumishi wa umma.
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa pamoja Zaina Mlawa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Robert Masunya wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu wajibu wao, hususan katika kuimarisha vita dhidi ya rushwa na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa.
Semina hiyo imeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye makao yake Mbeya.