Nuru FM

RC Kheri aagiza ununuzi wa bidhaa za ndani

21 July 2026, 08:50

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akiwa katika maonesho ya Nanenane Iringa. Picha na Hafidh Ally

RC Khei amesena kuwa matumizi ya bidhaa za ndani yataongeza kipato cha wazalishaji, kuchochea uundaji wa ajira, kuimarisha biashara na kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya Mkoa wa Iringa.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na viongozi wa taasisi za umma kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Iringa zinapewa kipaumbele katika ununuzi wa serikali, mradi zikidhi viwango vinavyohitajika.

Akifunga rasmi Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane ngazi ya Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika viwanja vya Kihesa Kilolo, Manispaa ya Iringa, Mhe. James amesema taasisi za umma pamoja na wananchi wanapaswa kuwa soko la kwanza la bidhaa zinazozalishwa ndani ya mkoa badala ya kutegemea bidhaa kutoka maeneo mengine.

Sauti ya Kheri

Aidha, Mhe. James ametangaza kuwa kuanzia Maonesho ya Nane Nane ya mwaka 2027, Mkoa wa Iringa utaanzisha mfumo wa ushindani utakaohusisha halmashauri, taasisi na waoneshaji binafsi kwa lengo la kuongeza ubunifu, kuboresha ubora wa maonesho na kuyafanya kuwa miongoni mwa maonesho bora nchini.

Sauti ya RC Kheri

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika tafiti za maji ya chini ya ardhi, uchimbaji wa visima na usimamizi bora wa rasilimali za maji ili kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sauti ya Munkyala

Awali, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Elias Luvanda, amesema maonesho ya mwaka huu yameleta mafanikio makubwa kwa kuwajengea wakulima, wafugaji na wavuvi uelewa kuhusu fursa za masoko, kupanua mitandao ya biashara na kuhamasisha usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani badala ya kuyauza yakiwa ghafi.

Alisema waoneshaji zaidi ya 100 walitoa elimu ya vitendo kwa wananchi kupitia teknolojia mpya za uzalishaji, huku wafanyabiashara wakibadilishana mawasiliano yaliyofungua fursa mpya za biashara.

Maonesho ya mwaka huu yaliwakutanisha waoneshaji 101 kutoka taasisi za umma na binafsi, kampuni za pembejeo, wakulima, wafugaji, wavuvi, taasisi za fedha na wajasiriamali. Wananchi walipata fursa ya kujifunza teknolojia mpya za uzalishaji, kufanya biashara na kujenga ushirikiano unaotarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi mkoani Iringa.