Kiwanda bubu cha pombe bandia chabainika Mafinga
31 August 2026, 09:28

Watu watatu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watafikishwa katika hatua za kisheria kwa kosa la kuzalisha pombe bandia.
Na Hafidh Ally
Kiwanda bubu kinachodaiwa kutengeneza pombe kali bandia kimebainika katika eneo la Pipeline, Mjini Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, baada ya operesheni iliyofanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.
Katika operesheni hiyo, watu watatu wamekamatwa pamoja na bidhaa mbalimbali na vifaa vinavyodaiwa kutumika katika uzalishaji wa vinywaji hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Selekwa, amesema miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni lita 90 za kimiminika kinachodaiwa kuwa pombe, chupa 144 za Konyagi, chupa 12 za Cuca Vodka pamoja na chupa saba za Roboti Gin.

Mhe. Selekwa amesema uwepo wa kiwanda hicho unahatarisha afya za walaji, kwa kuwa vinywaji hivyo vinatengenezwa katika mazingira yasiyozingatia usalama na havina nembo ya TBS inayothibitisha ubora na usalama wa bidhaa hizo.
Aidha, Mhe. Selekwa amesema watu watatu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watafikishwa katika hatua za kisheria, huku akitoa rai kwa wakazi wa Mafinga na Wilaya ya Mufindi kuwa waangalifu wanaponunua na kutumia vinywaji.
Amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha bidhaa wanazonunua zina nembo halali ya TBS na kutumia Scan Code ya TRA ili kuthibitisha uhalali wa bidhaa hizo na stempu za kodi.
Naye Meneja wa TRA Mufindi, Ndugu Mordekai Kibona, amesema kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wamekagua uhalali wa stempu za TRA zilizotumika kwenye vinywaji hivyo na kubaini kuwa ni bandia na hazikutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
