Kiswaga achangia Sh. 500,000 kwa umeme wa pampu Mangalali
10 September 2026, 14:19

Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga, amechangia Shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa umeme utakaotumika kuendesha pampu ya maji katika Kisima Kirefu cha Umeme, kilichopo Kijiji cha Mangalali, Kata ya Ulanda.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangalali, Bw. Kibadeni Mduda, amemshukuru Mbunge Kiswaga pamoja na Diwani wa Kata hiyo kwa ushirikiano na mshikamano wao katika kusukuma mbele miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini hapo.
Naye Diwani wa Kata ya Ulanda, Mhe. Philimone Temaigwe, amesema uwepo wa kisima hicho cha maji utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kijiji hicho.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mangalali wameeleza kuwa mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwao, kwani awali walikuwa wakikaa kwa muda mrefu bila kupata huduma ya maji, hali ambayo sasa imeanza kupungua kutokana na uwepo wa mradi huo.
Mradi huo wa maji, uliochimbwa na Shirika la Afya Plus, unalenga kuhudumia Kijiji cha Mangalali pamoja na vitongoji vyake nane.