Milioni 52.64 zajenga daraja la mto Mgega Mufindi
23 September 2026, 08:59

Kabla ya ujenzi huo, wananchi hao wamesema kuwa walipata adha kubwa baada ya daraja la awali kuharibika.
Na Hafidh Ally
Jumla ya shilingi milioni 52.64 zimetumika katika ujenzi wa Daraja la Mto Mgega, linalounganisha Kijiji cha Mwilavila na Isimikini, Kata ya Malangali, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, wilayani Mufindi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu, Maendeleo ya Miji na Vijijini wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mhandisi Said Kachenje, amesema ujenzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu na kurahisisha maisha ya wananchi, hususan maeneo ya vijijini.
Akizungumza baada ya kukagua daraja hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mkazo katika uwekezaji wa miundombinu, kwa kuwa barabara na madaraja ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji na mawasiliano, hivyo kuchochea shughuli za maendeleo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu, akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto mbalimbali za msingi zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Malangali wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo, wakisema awali walikabiliwa na adha kubwa baada ya daraja la zamani kuharibika.
Wamesema hali hiyo ilisababisha usafiri kuwa mgumu, hasa wakati wa mvua, na wakati mwingine kuwaathiri wanawake wajawazito waliokuwa wakihitaji kufika kwa wakati katika vituo vya afya.
