Kiswaga achangia Mil 1.5 kusaidia Kaya 12 zilizoathiriwa na Mvua Magulilwa
24 October 2026, 14:12

Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ametoa Sh1.5 milioni kusaidia kaya 12 zilizoathirika na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika Kata ya Magulilwa, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa.
Mvua hiyo iliyonyesha Oktoba 21, 2026, katika Kijiji cha Ng’enza, ilisababisha nyumba kuezuliwa mapaa, vyakula kulowa na familia kukosa makazi salama katika vitongoji vya Lutengelo na Muungano.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mbunge, Katibu wake, Yustini Mgao, amewapa pole waathirika na kusema msaada huo unalenga kuwafariji katika kipindi hiki kigumu, huku akihimiza mshikamano katika kuwasaidia kurejesha maisha yao ya kawaida.
Diwani wa Kata ya Magulilwa, Boaz Mbilinyi, ameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa msaada huo na kutoa wito kwa wadau, taasisi na watu wenye uwezo kujitokeza kusaidia waathirika, hasa katika upatikanaji wa makazi na mahitaji muhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’enza, Amatus Kindole, amesema mvua hiyo imewaweka baadhi ya wananchi katika mazingira magumu kutokana na kuharibika kwa nyumba na kulowa kwa vyakula vilivyohifadhiwa majumbani, akieleza kuwa kijiji hicho hakijawahi kushuhudia athari za kiwango hicho.
Miongoni mwa walioathirika ni Elizabeth Ngailevanu, mjane mwenye watoto wanne, ambaye nyumba yake iliezuliwa na upepo na bati kuharibika, hali iliyosababisha vyakula vyake kulowa. Ameomba wadau wengine kujitokeza kumsaidia kurejesha makazi yake na kuhakikisha watoto wake wanapata hifadhi salama.
Naye Mtendaji wa Kata ya Magulilwa, Merad Mpulule, amesema Serikali inaendelea kufuatilia hali ya waathirika na kuwataka wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika ili kujikinga na madhara ya mvua, huku wakitoa taarifa mapema kwa viongozi wanapoona viashiria vya hatari.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na viongozi pamoja na wadau mbalimbali katika kusaidia kaya zilizoathirika, akieleza kuwa usalama wa maisha na mali unapaswa kupewa kipaumbele wakati huu wa mvua zinazoambatana na upepo mkali.