Nuru FM

RC Kheri: “Usalama wa waandishi wa habari ni muhimu kwa maendeleo”

3 November 2026, 08:38

“Usalama wa waandishi wa habari haupaswi kuangaliwa kama suala la taaluma pekee, bali pia kama sehemu ya mkakati mpana wa maendeleo ya taifa” Kheri

Na Adelphina Kutika

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema usalama wa waandishi wa habari ni jambo muhimu katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uhuru na weledi, akisisitiza kuwa mchango wa tasnia ya habari katika maendeleo ya taifa unaweza kuwa hatarini endapo waandishi watakabiliwa na vitisho, ukatili au vikwazo visivyo vya lazima.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe.Kheri James katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Ukosefu wa Adhabu kwa Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari, yaliyoandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Sauti ya Kheri

Kheri James amesema waandishi wa habari wanapaswa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi, zilizothibitishwa na zenye uwiano, huku akieleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kuibua changamoto na kuhabarisha wananchi kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini.

Sauti ya Kheri

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Erenest Sungura, amesema matukio 12 ya ukiukwaji dhidi ya waandishi wa habari yamethibitishwa mwaka 2026 hadi sasa, ikilinganishwa na matukio 51 yaliyoripotiwa mwaka 2025 ambayo yanahusisha kukamatwa kwa waandishi wa habari na kunyang’anywa vifaa vyao vya kazi.

Sauti ya Sungura

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya MCT, Yusuph Khamis Yusuph, amesisitiza umuhimu wa viongozi na wadau mbalimbali kuheshimu kazi za waandishi wa habari, akieleza kuwa uwazi na uwajibikaji ni muhimu katika kuimarisha usalama wa wanahabari.

Sauti ya Yusuph