Nuru FM

Shamba la Kibidula kuongeza uzalishaji wa parachichi hadi tani 120 kwa siku

28 October 2026, 10:44

Mkurugenzi wa Shamba la Kibidula, Jason Fournier akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Picha na Hafidh Ally

Shamba hilo limeajiri wafanyakazi 263 na kuchangia zaidi ya shilingi bilioni moja katika mapato ya kodi

Na Hafidh Ally

Uongozi wa Shamba la Parachichi la Kibidula lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, mkoani Iringa, umesema unatarajia kuongeza uzalishaji wa parachichi kutoka tani 48 kwa siku hadi tani 120 kwa siku katika mwaka wa fedha wa 2026/2027.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, wakati wa ziara ya kutembelea viwanda mkoani humo, Mkurugenzi wa Shamba la Kibidula, Jason Fournier, amesema uzalishaji wa parachichi umekuwa ukiongezeka kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Amesema shamba hilo limeajiri wafanyakazi 263 na kuchangia zaidi ya shilingi bilioni moja katika mapato ya kodi kwa mwaka wa fedha uliopita.

Sauti ya Jason
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza katika shamba la Parachichi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema amefurahishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa katika shamba hilo, akieleza kuwa ubora huo unachangia kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani na kimataifa.

Sauti ya RC Kheri

Aidha, Kheri amesisitiza umuhimu wa jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji kunufaika na uwepo wa wawekezaji, huku akiwataka wananchi kudumisha uaminifu na uadilifu ili kuimarisha ushirikiano na kuendeleza uwekezaji huo.

Sauti ya RC Kheri

Shamba la Kibidula lina ukubwa wa zaidi ya ekari 4,000 na lina kiwanda cha kisasa cha kufungasha parachichi (packhouse), kinachowezesha maandalizi ya zao hilo kwa ajili ya kusafirishwa na kuuzwa katika masoko mbalimbali.