Nuru FM

RC Iringa awataka wananchi kulinda mradi wa umeme wa upepo Mufindi

27 October 2026, 09:39

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri james akiwa katika ziara ya kikazi Wilaya ya Mufindi. Picha na Hafidh Ally

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 50 unatajwa kuwa sehemu ya uwekezaji katika sekta ya nishati unaolenga kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi huo.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka viongozi wa vijiji vinavyozunguka mradi wa umeme wa upepo uliopo Kijiji cha Usokami, Wilaya ya Mufindi, kuhamasisha wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 3.9.

Akizungumza wakati wa kutembelea mradi huo katika ziara yake ya siku tano ya kukagua viwanda mkoani Iringa, Mhe. Kheri amesema mradi huo una manufaa kwa wananchi zaidi ya elfu tisa kutoka vijiji 32 vilivyopo katika kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Sauti ya RC Kheri

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuutunza mradi huo ili uendelee kutoa huduma ya umeme na kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya jamii.

Sauti ya RC Kheri

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Mwenge Hydro Power Limited, Deogratius Massawe, amesema kampuni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara.

Sauti ya Meneja Massawe

Naye Michael Mahenge, akizungumza kwa niaba ya wananchi wanufaika, amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa kurahisisha shughuli za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme.

Sauti ya Mwananchi

Amesema upatikanaji wa umeme umewawezesha wananchi kuanzisha shughuli ndogo za uzalishaji, ikiwemo kusaga mahindi, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kufungua fursa za kuongeza kipato.