Nuru FM

RC Kheri aagiza mkakati wa vijana kupata mafunzo kwa vitendo

28 November 2026, 08:14

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James akizungumza katika Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU). Picha na Adelphina Kutika

Utoaji wa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu unajenga rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na uzoefu unaohitajika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Na Adelphina Kutika

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameiagiza Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa kwa kushirikiana na RUCU na vyuo vingine vya elimu ya juu kuweka mkakati utakaowawezesha vijana kupata mafunzo kwa vitendo katika taasisi mbalimbali za serikali na sekta nyingine.

Agizo hilo limetolewa wakati wa Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU), ambapo amesema mpango huo utawasaidia vijana kupata uzoefu wa kazi, kuongeza ujuzi na kuwa na ushindani katika soko la ajira.

Amesema kuwapa vijana nafasi ya kufanya kazi kwa vitendo chini ya usimamizi wa wataalamu kutawajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za mazingira halisi ya kazi.

Sauti ya RC Kheri

Mhe. Kheri amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inahitaji vijana wenye uwezo wa kutumia elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa vyuoni kuunganishwa na mazingira halisi ya kazi ili kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha, Prof. Chrispina Lekule, amewataka wahitimu kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha, bali kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni kubuni fursa za kiuchumi na kujiajiri.

Sauti ya Prof. Chrispina Lekule

Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu wameeleza kuwa elimu waliyoipata itakuwa msingi wa kujiajiri, kuchangia maendeleo ya jamii na kutumia taaluma zao kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Sauti ya Wahitimu