Wahitimu wa Pomerini wakabidhi madawati 30 shule waliyosoma
16 October 2026, 09:59

Na Joyce Buganda
Wahitimu wa Shule ya Sekondari Pomerini waliomaliza kidato cha nne mwaka 1994 na 1995 wamekabidhi madawati 30 yenye thamani ya shilingi milioni 1.5 kwa shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha shukrani kwa shule waliyosomea.
Wakizungumza mbele ya wanafunzi shuleni hapo, baadhi ya wahitimu hao wamesema madawati hayo yamepatikana kupitia michango ya wahitimu wa miaka hiyo, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
Kwa niaba ya wanafunzi, kaka mkuu wa shule hiyo amewashukuru wahitimu hao kwa msaada walioutoa, huku akiahidi kuwa yeye na wanafunzi wenzake watasoma kwa bidii ili kufikia ndoto na malengo waliyojiwekea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Pomerini, Mwalimu Edwin Makongwa, amewashukuru wahitimu hao kwa kuikumbuka shule yao na kutoa mchango huo, akisema madawati hayo yatasaidia kuboresha mazingira ya kukaa na kujifunzia kwa wanafunzi.
