Kiswaga akabidhi mifuko 100 ya saruji Magunga
13 July 2026, 10:21

“Nitaendelea kuwaunga mkono wananchi ili kuhakikisha miradi muhimu inakamilika kwa wakati na kuleta huduma bora kwa jamii”
Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga, ameendelea kuunga mkono juhudi za wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya kukabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Kiswaga alisema msaada huo ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha mazingira ya kazi na makazi ya watumishi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali katika kufanikisha miradi ya maendeleo.
Alieleza kuwa hiyo si mara ya kwanza kuchangia mradi huo, kwani awali alitoa bati 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo. Aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi hadi mradi huo utakapokamilika.
“Mafanikio ya miradi ya maendeleo yanategemea ushirikiano wetu sote. Nitaendelea kuwaunga mkono wananchi ili kuhakikisha miradi muhimu inakamilika kwa wakati na kuleta huduma bora kwa jamii,” alisema Mhe. Kiswaga.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Michael Mgimwa, alimpongeza Mbunge Kiswaga kwa mchango huo, akisema utasaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba hiyo. Alieleza kuwa wananchi wameweka lengo la kuukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Oktoba ili kuwaondolea changamoto watumishi ambao kwa sasa wanaishi katika nyumba za kupanga kutokana na uhaba wa makazi ya watumishi.
Mbali na kukabidhi vifaa vya ujenzi, Mhe. Kiswaga alipata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kijiji hicho. Kero iliyopewa uzito zaidi ilikuwa migogoro ya ardhi, ambapo wananchi walidai kuwa mwekezaji mmoja amechukua sehemu ya ardhi yao kinyume na taratibu, jambo ambalo walisema limeathiri shughuli zao za kiuchumi na ustawi wa maisha yao.
Wananchi walitoa wito kwa Serikali kuingilia kati ili kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Mhe. Kiswaga aliwahakikishia wananchi kuwa atashirikiana na mamlaka zinazohusika kufuatilia suala hilo ili lipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Hatua hiyo imepokelewa kwa matumaini na wananchi wa Magunga, ambao wamesema ushirikiano kati ya viongozi na jamii ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili.
