Polisi Iringa yawakamata watuhumiwa 215
12 June 2026, 08:53

Katika operesheni zinzaofanywa na Jeshi la Polisi walifanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodhaniwa kuwa za wizi Mkoani Iringa.
Na Hafidh Ally
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewakamata watuhumiwa 215 kwa makosa mbalimbali katika kipindi cha Mei 1 hadi Juni 9, 2026 kupitia misako, doria na operesheni maalumu zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu na kulinda usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, huku watuhumiwa hao wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika operesheni hizo, polisi walifanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodhaniwa kuwa za wizi zikiwemo magari mawili aina ya Toyota Alteza na Toyota Rav4, mapipa 104 ya lami, vipande 200 vya marine board, runinga mbili, redio nane aina ya subwoofer, simu saba za mkononi, pikipiki saba, kompyuta mpakato mbili, magodoro mawili, mitungi mitatu ya gesi pamoja na vifaa vingine vya matumizi ya nyumbani.

Kamanda Bukumbi amesema Juni 9, 2026 polisi walifanya ukaguzi katika kizuizi cha magari eneo la Igumbilo, Manispaa ya Iringa na kuwakamata watu wanne waliokuwa wakisafirisha katoni 177 za vipodozi aina mbalimbali vya mafuta ya kupaka vilivyopigwa marufuku nchini.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, vipodozi hivyo vilikutwa ndani ya basi la Kampuni ya Royale lenye namba za usajili T701 CBR aina ya Scania lililokuwa likitokea Zambia kuelekea Dar es Salaam, huku hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao zikiendelea kuchukuliwa.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa lilimkamata dereva Iddi Jumanne Shija, mkazi wa Dar es Salaam, baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiendesha gari kwa njia hatarishi katika Kijiji cha Mtandika wilayani Kilolo.

Kwa upande mwingine, jumla ya washtakiwa 155 wamehukumiwa vifungo mbalimbali kwa makosa tofauti, yakiwemo ubakaji, kupatikana na nyara za Serikali pamoja na makosa mengine ya jinai.