Wananchi Ihongole wachimba mtaro kwa ajili ya mradi wa maji
17 August 2026, 09:09

Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Mtaa wa Ihongole, Halmashauri ya Mji Mafinga, wamejitolea kuchimba mtaro na kupokea vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji unaosimamiwa na Shirika la People Development Forum (PDF), kwa lengo la kusambaza huduma ya maji ya bomba katika eneo hilo.
Wakizungumza wakati wa kushiriki shughuli hiyo ya maendeleo inayolenga kufikisha huduma ya maji katika Shule ya Msingi Mwongozo, baadhi ya wananchi wamesema wameamua kujitolea kuchimba mtaro ili kurahisisha uwekaji wa mabomba na hatimaye huduma ya maji kuwafikia wananchi na wanafunzi.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Mwongozo, Atu Mng’ong’o, amewashukuru wazazi na wananchi kwa kujitolea kufanya kazi za mikono, akisema hatua hiyo itarahisisha huduma ya maji kufika shuleni hapo na kupunguza changamoto ya wanafunzi kufuata maji wakati wa masomo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Boma, Baraka Kisakanike, amesema mradi huo utasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mtaa wa Ihongole.
Aidha, Diwani Kisakanike amesema huduma hiyo itawanufaisha wananchi wa kata hiyo, huku akilishukuru Shirika la People Development Forum (PDF) pamoja na Serikali kwa kushirikiana katika utekelezaji wa mradi huo.
