Kihorogota FC yatwaa ubingwa wa Mgongolwa super Cup 2026
28 September 2026, 11:33

Na Hafidh Ally
Timu ya Kihongorota Fc imefanikiwa kuwa mabingwa wa Mashindano ya Mgongolwa super cup baada ya kuifunga Ivangwa FC Goli 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Isiman Tarafani.
Mara baada ya Kihorogota Fc kutawazwa mabingwa wa Mashindano hayo, wamepatiwa Zawadi ya Ng’ombe Mwenye thamani ya shilingi laki nane na Jezi Seti Moja, huku mshindi wa Pili Ivangwa Fc akipata zawadi ya Mbuzi wawili na Jezi seti moja na Mshindi wa Tatu Ndolela FC akipewa zawadi ya Mbuzi mmoja na Jezi seti Moja.
Akizungumza wakati wa kuhimisha mashindano hayo, Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini, Anold Mvamba amempongeza Diwani wa Kata hiyo Michael Mgongolwa kwa kuanzisha mashindano hayo na kutoa zawadi kwa washindi wote.

Aidha amesema kuwa katika mashindano yajayo, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Isiman Emmanuela Mtatifikolo itashirikiana naye katika kuratibu mashindano ngazi ya Jimbo ili kukuza vipaji vya vijana.

Awali Diwani wa Kata hiyo Michael Mgongolwa amesema kuwa wakati anaanzisha mashindano hayo aliwasiliana na Mbunge wa Jimbo la Isiman na aliamua kuchangia zawadi kwa kutoa jezi kwa washindi wa mashindano hayo.
“Kwa kuhakikisha Kata ya Kihorogota inaendelea kung’ara, mashindano haya yameungwa mkono pia na Mbunge wetu wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda,” alisema Mgongolwa.
Naye Mratibu wa mashindano Elieza Dononda hayo alisema mashindano hayo yalishirikisha timu nane tangu yalipoanzishwa na yalikuwa na lengo la kutoa nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.

Naye Nahodha wa Kihoroga FC Justine Lyabula amesema kuwa mashindano yalikuwa mazuri na kulikuwa na ushindani licha ya wao kujipanga na kuchukua ubingwa huku nahodha wa Ivangwa FC Hamadi akikiri kuwa walikuwa na changamoto katika umaliziaji wa nafasi walizozitengeneza.
Mashindano hayo ya Mgongolwa Super Cup 2026 yalishirikisha timu nane na yalifikia tamati katika Kata ya Kihorogota, huku viongozi wakimpongeza Diwani wa Kata hiyo, Michael Mgongolwa, kwa kuanzisha mashindano hayo kwa lengo la kukuza vipaji na kuhamasisha vijana kushiriki michezo.
