Meya Iringa aagiza kudhibiti bei ya nyama
27 November 2026, 16:38

Na Aldephina Kutika
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahimu Ngwada, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kukutana na wafanyabiashara wa nyama kujadili kupanda kwa bei ya nyama kutoka Shilingi 10,000 hadi Shilingi 12,000 kwa kilo.
Agizo hilo amelitoa wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Fabiani Ngajilo, katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Robo ya Kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Iringa.
Katika swali lake, Ngajilo alitaka kujua sababu za kupanda kwa bei ya nyama mkoani Iringa licha ya mkoa huo kuwa na wafugaji wengi.

Akijibu swali hilo, Ngwada amesema ni muhimu Mkurugenzi kukutana na wafanyabiashara wa nyama ili kubaini changamoto zinazosababisha kupanda kwa bei hiyo na kutafuta suluhisho litakalowezesha wananchi kupata nyama kwa gharama wanazoweza kumudu.
Ameeleza kuwa kupanda kwa bei ya nyama kunaweza kuwafanya baadhi ya wananchi, hususan wenye kipato cha chini, kushindwa kumudu mlo wenye nyama na kulazimika kutegemea vyakula vingine kama maharagwe.
Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wa nyama huku ikihakikisha maslahi ya wananchi na uwezo wao wa kumudu gharama za maisha vinazingatiwa.
