RC Kheri awataka vijana Iringa kuikataa rushwa
7 September 2026, 10:01

Elimu ya kupinga rushwa ni muhimu katika kuwaandaa vijana ambao watakuwa viongozi waadilifu na wenye uzalendo katika siku zijazo.
Na Hafidh Ally
Vijana Mkoani Iringa wametakiwa kuikataa na kuichukia rushwa pamoja na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo, ili kujenga taifa imara lenye haki na usawa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, wakati akifungua Mdahalo wa Wapinga Rushwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutoka mikoa ya Dodoma na Iringa, uliofanyika katika Shule ya Sekondari Lugalo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Mhe. Kheri amesema vitendo vya rushwa vimekuwa vikisababisha baadhi ya watu kukosa fursa mbalimbali, kutokana na baadhi ya watu kutumia rushwa kuwapa nafasi watu wasio na sifa au wasiostahili ambapo hali hiyo inapaswa kukomeshwa kwa kuwajenga watoto tangu wakiwa shuleni, ili wawe na uelewa wa madhara ya rushwa na kuwa tayari kuikataa.
Aidha, Mhe. Kheri amewataka walimu na wazazi kuhakikisha watoto wanalelewa na kufundishwa misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji, akisisitiza kuwa taifa linahitaji kizazi chenye maadili mema na malezi bora kitakachoweza kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa upande wake, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swela, amesema lengo la kuanzishwa kwa klabu za kupinga rushwa shuleni ni kuwapatia wanafunzi elimu kuhusu rushwa, madhara yake na namna ya kuikataa, ili kuwaandaa vijana watakaokuwa viongozi waadilifu siku zijazo.

Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika mdahalo huo wamepongeza uwepo wa klabu za kupinga rushwa shuleni, wakisema kuwa klabu hizo zinawasaidia kupata uelewa kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuwa waadilifu.
Mdahalo huo umewakutanisha zaidi ya wanafunzi 250 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari za mikoa ya Dodoma na Iringa.