Nuru FM

MUCE yakuza Tafiti na ubunifu Iringa

3 June 2026, 10:18

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Utafiti ,Ubunifu na huduma kwa jamii. Picha Na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Zaidi ya shilingi milioni 300 zimewekezwa na Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) katika kuendeleza mawazo bunifu na tafiti mbalimbali zenye lengo la kuzalishwa kibiashara na kutoa suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi nchini.

Hayo yameelezwa na Rasi wa chuo hicho Prof. Method Semiono, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utafiti ,Ubunifu na huduma kwa jamii yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (MUCE) katika viwanja vya Garden Mansipaa ya Iringa na kuongeza kuwa uwekezaji huo unalenga kuwezesha bunifu zinazozalishwa na watafiti kufikia hatua ya kuwa bidhaa zinazoweza kutumika na wananchi na kuuzwa sokoni.

Sauti ya Prof. Method

Prof. Semiono amesema maadhimisho hayo yanayokutanisha vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau mbalimbali yanaendana na azma ya kuimarisha ushirikiano kati ya elimu, viwanda na biashara ili kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia.

Amesema miongoni mwa bunifu zinazofanyiwa kazi ni mradi wa kubadilisha ulanzi, unaopatikana kwa wingi mkoani Iringa, kwa matumizi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, viwandani na matumizi mengine yenye thamani ya kiuchumi.

Rasi wa Chuo cha MUCE Prof. Method Semiono akizungumza katika Maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, Amesema amevutiwa na utafiti ulioonesha namna ulanzi unavyoweza kutumika kutengeneza bidhaa zinazohitajika katika sekta ya afya,hatua ambayo inaweza kufungua masoko mapya kwa wazalishaji na kuongeza mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.

Sauti ya RC Kheri

“Matokeo ya tafiti hizi yanaonesha wazi kuwa rasilimali tulizonazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha maendeleo endapo zitatumika kwa ubunifu na kuongeza thamani ni wajibu wetu kuendelea kuwekeza katika tafiti na teknolojia ili kuzalisha bidhaa zenye ushindani na manufaa kwa jamii,” Alisema Kheri

Aidha Mkuu wa Mkoa huyo Kheri amempongeza Rasi wa Chuo Kishiriki cha Mkwawa (MUCE), Prof. Method Semiono, kwa kuendelea kusimamia na kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutoa suluhisho la changamoto za maendeleo katika jamii.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa kaulimbiu isemayo: “Kutumia Utajiri wa Madini wa Tanzania kwa Nishati Jadidifu, Mabadiliko ya Kidijitali na Maendeleo ya Jamii.”