Ihongole kuweka historia ya kupata huduma ya maji kwa mara kwanza
2 August 2026, 10:33

Mradi huo Utaenda kuondoa changamoto ya Maji kwa wananchi wa Kijiji cha Ihongole.
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Kijiji cha Ihongole, kilichopo Kata ya Boma katika Halmashauri ya Mji Mafinga, wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa maji ya bomba utakaowafikia kwa mara ya kwanza katika historia ya kijiji hicho.
Diwani wa Kata ya Boma, Mheshimiwa Baraka Kisakanike, amewataka wananchi kuupokea mradi huo kwa moyo chanya na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake kwa kujitolea nguvu kazi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.

Awali, akitambulisha mradi huo wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji, Afisa Mradi kutoka Shirika la People Development Forum (PDF), Agnes Erio, alitoa maelezo kuhusu malengo, utaratibu na namna mradi utakavyotekelezwa.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia Maji na kutunza vyoo ili kujiepusha na maradhi ya mlipuko ambayo husabishwa na kutozingatia usafi.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi wa PDF, Mohamed Shaban Chuwa, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo, kutunza mazingira na kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo bora ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihongole, Patrick Kigodi, amewahimiza wananchi kushirikiana katika kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo ili uweze kutoa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muongozo, Atu Mung’ong’o, alilishukuru Shirika la PDF kwa kufikisha mradi huo kijijini na kutoa wito kwa wazazi kushiriki katika kuboresha hali ya usafi wa mazingira, akibainisha kuwa shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyoo bora.