Nuru FM

RC Kheri atatua mgogoro wa ardhi Magubike

30 April 2026, 10:05

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akizungumza katika kijiji cha Magubike. Picha na Ayoub Sanga

Mgogoro huo ulipelekea Bw. Mpambe Mnyambeyu, kuzuiwa kufanya shughuli za kimila katika makaburi ya wazazi wake yaliyopo ndani ya eneo la mgogoro, hatua inayotajwa kuleta suluhu na kurejesha amani kwa pande zinazosigana.

Na Ayoub Sanga

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka minne ukimuhusisha Mpambe Thomas, mkazi wa Kijiji cha Magubike, Kata ya Nzihi na kampuni ya uwekezaji ya Premium Active Tanzania Ltd juu ya umiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya elfu 1.

Akizungumza wakati wa mkutano wa usuluhishi uliowakutanisha wananchi, muwekezaji na mlalamikaji huyo katika Kijiji cha Magubike, Mhe. Kheri James amesema lengo la serikali ni kuhakikisha pande zote zinapata haki na kuridhika ili kudumisha amani na kuchochea maendeleo katika eneo hilo.

Sauti ya RC Kheri

Katika uamuzi wa serikali, Kupitia Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amebainisha kuwa Mlalamikaji Mpambe Thomas ameruhusiwa kumiliki na kutumia eneo la makaburi ya mababu zake pamoja na kufanya shughuli zake za kimila ikiwemo matambiko ambapo Serikali imeondoa eneo hilo katika hati ya muwekezaji.

Sauti ya RC Kheri

Hata hivyo, Bw. Thomas alipinga umiliki huo akieleza kuwa eneo hilo linamilikiwa na familia yake kwa muda mrefu, na lina makaburi ya mababu zake ambapo aligundua uwepo wa hati rasmi ya eneo hilo baada ya benki kufika eneo hilo kutoa taarifa kuhusu umiliki wa ardhi hiyo.

Sauti ya Thomas

Kupitia mamlaka ya kijiji, mlalamikaji amepewa eneo la ekari 8 kwa ajili ya matumizi yake binafsi, hatua inayolenga kumuwezesha kuendelea na shughuli zake za kijamii na kiuchumi.

Kampuni ya Premium Active Tanzania Ltd inamiliki eneo hilo baada ya kuuziwa na mtu mwingine ambaye alikuwa mwekezaji kwenye eneo hilo kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2 baada ya mwekezaji huyo kukopa Benki fedha kwa kutumia hati ya eneo hilo na aliposhindwa kulipa mkopo ndipo Benki ilifikia maamuzi ya kulipiga mnada eneo hilo ambalo ndani yake lilikuwa na vitu kama makaburi ya wazazi wa Mpambe Mnyambeyu.