Nuru FM
Nuru FM
3 March 2026, 09:50

Mkitaka kukopa ni vyema mkazifuata taasisi zinazotoa mikopo zilizosajiliwa kisheria
Na Fredrick Siwale
Wanawake Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa wametakiwa kutojihusisha na mikopo yenye viashiria vya kausha damu ili ambayo imekuwa ikileta taharuki na kupoteza utu wa mwanamke pindi wanaposhindwa kurejesha.
Hayo yamezungumzwa wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Mufindi Bi. Mercheline Mkini iliyoadhimishwa ngazi ya Kata ya Ikongosi na Mtili na kuongeza kuwa ni vyema wanapokopa kuwashirikisha wenza wao ili wajue mikopo hiyo inatumikaje.

“Mikopo ina faida na hasara muhimu shirikisheni Wenza wenu na sio kukopa kinyemela. ” Alisema Bi. Mkini.
Kwa upande wao Diwani wa Viti maalum Kata ya Ikongosi Mh. Magreth Kaguo na Diwani wa Viti maalum Kata ya Ifawagi Mh. Beatrice Mpwagi wamesema kuwa wanawake wanapaswa kukopa kwa ajili ya kufanya biashara ili fedha hizo zizalishe na kujikwamua kiuchumi.
Awali wake Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Iringa kupitia kundi la Vijana Taifa, Mh. Jasmine Ng’umbi ametoa rai kwa Wanawake kusimama kutumia fursa za mikopo katika taasisi zinazotambulika ili waweze kufanya maamuzi ya kujiendeleza kiuchumi.
Kwa upande wao Maafisa kutoka Benki ya Mucoba Bi Amina Mkongimi ambaye ni Kaimu Meneja Udeshaji wa Benki ya Mucoba na Mary Mpwaga Afisa mikopo wa Benki hiyo wametoa ushauri kwa jamii pindi wanapotaka kukopa kwa ajili ya biashara ni lazima wafanye tathmini ya kile wanachotaka kukifanya.