Nuru FM

RC Kheri awataka watumishi wapya kuzingatia maadili

28 July 2026, 09:52

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza na Watumishi wapya Mkoani Iringa. Picha na Hafidh Ally

Mhe. Kheri amewahimiza watumishi hao kuwa waadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma, kuwajibika kwa matendo yao na kuendelea kujiimarisha kiuchumi kupitia matumizi sahihi ya kipato chao ili kujenga maisha yenye utulivu na kuongeza tija katika utendaji wao wa kazi.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka watumishi wapya waliopangiwa kazi katika taasisi mbalimbali za umma mkoani Iringa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia ushirikiano, uadilifu na heshima kwa wananchi pamoja na watumishi wenzao ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.

Akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa kikao cha kuwakaribisha na kuwapa maelekezo watumishi hao, Mhe. Kheri amesema mkoa huo umepokea watumishi wapya 200 watakaosaidia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Sauti ya Kheri

Aidha, Mhe. Kheri amewataka watumishi hao kujenga utamaduni wa uwazi, usawa na ushirikiano mahali pa kazi, huku wakihakikisha wanatoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wananchi. Amesisitiza kuwa maadili mema ya utumishi wa umma ndiyo msingi wa kujenga imani ya wananchi kwa Serikali.

Sauti ya Kheri

Vilevile, amewahimiza watumishi hao kuwa waadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma, kuwajibika kwa matendo yao na kutumia ipasavyo kipato chao ili kujiimarisha kiuchumi, kujenga maisha yenye utulivu na kuongeza tija katika utendaji wa kazi.