Wananchi Malangali kuanza kupata huduma za mionzi
24 September 2026, 09:23

Ujenzi wa jengo hilo la huduma za mionzi katika Kituo cha Afya Malangali, linajengwa kwa lengo la kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.
Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kata ya Malangali na maeneo ya jirani wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa jengo la huduma za mionzi katika Kituo cha Afya Malangali, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wakisema awali walilazimika kutembea na kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 20 kwenda Hospitali ya Wilaya kufuata huduma hiyo.
Wananchi hao wamesema Hayo mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James kukagua mradi huo ambapo wamesema kukamilika kwa jengo hilo kutawarahisishia upatikanaji wa huduma za mionzi kwa kuwa hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu, hatua ambayo wameeleza itasaidia kupunguza gharama na changamoto wanazokutana nazo wanapohitaji huduma hiyo.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Malangali amesema kukamilika kwa jengo hilo kutawanufaisha wananchi wapatao 6,331 wa Kata ya Malangali na maeneo ya pembezoni akisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 58 kimetumika.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amesema kuwa huduma ya mionzi imekuwa ikihitajika na wananchi wengi, hivyo Serikali imeamua kuwekeza katika huduma hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao badala ya kusafiri umbali mrefu.
Aidha Mhe. Kheri amewataka wahusika kuhakikisha sehemu zilizobaki za ujenzi zinakamilishwa kwa wakati ili jengo hilo lianze kutoa huduma kwa wananchi huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma itakayotolewa katika kituo hicho inakuwa bora na yenye kukidhi mahitaji ya wananchi wa Malangali na maeneo ya jirani.
