Pomerini FC yaibuka mabingwa wa Mwl Mlyuka Super cup 2026
19 October 2026, 12:07

Na Rashid Lihoha na Hafidh Ally
Timu ya Pomerini FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mlyuka Super Cup 2026 baada ya kuifunga Torino FC bao moja kwa sifuri katika mchezo wa fainali uliofanyika katika Kijiji cha Pomerini, Kata ya Ng’uruhe, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Kwa ushindi huo, Pomerini FC imezawadiwa mbuzi, seti moja ya jezi, mpira na shilingi elfu hamsini, huku Torino FC, iliyomaliza nafasi ya pili, ikipata seti moja ya jezi, mipira na shilingi elfu thelathini.
Katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Kihesa Mgogao iliifunga Lukani FC mabao mawili kwa sifuri. Kihesa Mgogao ilipata mpira na shilingi elfu thelathini, huku Lukani FC ikipata shilingi elfu thelathini.
Kwa upande wa mchezo wa netiboli, timu ya Pomerini iliibuka mshindi dhidi ya timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kujinyakulia zawadi ya shilingi elfu arobaini.

Akizungumza baada ya fainali hiyo, mdhamini wa mashindano hayo, Mwalimu Francis Mlyuka, amesema lengo la mashindano hayo ni kuwaunganisha vijana, kukuza vipaji vyao, kuwaepusha na vitendo hatarishi na kuimarisha amani nchini.
Mlyuka amewashukuru wadau waliofanikisha mashindano hayo, akieleza kuwa yamefanikiwa kwa asilimia mia moja na kwamba yatafanyika kila mwaka.

Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Bahati Nyambaga, amewahimiza wananchi kushiriki mbio za Kitonga Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Naye Lucy Mbuma amesema Kitonga Marathon inalenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa maliasili za Mlima Kitonga, kutangaza fursa za uwekezaji na kukuza utalii wa asili pamoja na utalii wa michezo.
Mbali na soka na netiboli, fainali hizo zilipambwa na michezo mingine ikiwemo voliboli, kukimbia ndani ya magunia, kukimbia na yai kwenye kijiko, kubeba chupa kichwani, michezo ya jadi na mashindano ya kula na kunywa.
