Nuru FM

Dkt. Chaya apongeza uwekezaji wa ASAS dairies Iringa

24 November 2026, 09:54

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya akizungumza wakati wa ziara katika kiwanda cha ASAS. Picha na Hafidh Ally

Kiwanda cha Asas kimetoa ajira kwa zaidi ya watu 400, ambapo asilimia 60 ni wanawake, hatua inayochangia kuwawezesha kiuchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Na Hafidh Ally

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amepongeza uwekezaji uliofanywa na Kiwanda cha ASAS Dairies mkoani Iringa, akisema umechangia kuongeza thamani ya maziwa, kukuza sekta ya mifugo na kupanua fursa za ajira kwa vijana na wanawake.

Dkt. Chaya ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Iringa, ambapo ametembelea kiwanda hicho kilichopo mjini Iringa kujionea shughuli za uzalishaji, uwezo wa kiwanda pamoja na mchango wake katika kukuza uchumi.

Amesema uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ni muhimu katika kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha mnyororo wa uzalishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutambua fursa na changamoto zinazowakabili wawekezaji.

Sauti ya Dkt. Chaya Naibu Waziri

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kutambua mahitaji ya wawekezaji na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea uwekezaji, kuongeza uzalishaji na ajira pamoja na kukuza uchumi wa mkoa na taifa.

Sauti ya Dkt. Chaya Naibu Waziri

Naye mmoja wa wakurugenzi wa Kiwanda cha ASAS Dairies, Ahmed Asas, amesema sekta binafsi ina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo, ikiwemo kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Sauti ya Ahmed Asas

Ziara hiyo inalenga kutathmini hali ya uwekezaji mkoani Iringa, kubaini fursa zilizopo na changamoto zinazowakabili wawekezaji, ili kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.