Nuru FM

Viongozi wa timu shiriki Kiswaga cup 2023 wapewa semina

20 August 2023, 1:09 pm

Baadhi ya Viongozi wa timu shiriki Kiswaga cup 2023 wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Semina. Picha na Hafidh Ally

Semina hiyo imelenga kuwapa kanuni na sheria za mashindano ya Kiswaga Cup ili kuepukana na changamoto za kikanuni.

Na Hafidh Ally

Viongozi wa timu shiriki katika mashindano ya Kiswaga cup 2023 yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Kalenga Mh Jackson Kiswaga wamepewa semina elekezi kwa ajili ya kujua kanuni na sheria za mashindano hayo.

Semina hiyo iliyojikita kwenye kanuni za mashindano na sheria za Mpira wa Miguu imetolewa na Mwamuzi Mkongwe Rashid Zongo (Shungu) katika ukumbi wa Misheni uliopo Kijiji Cha Nyabula.

Akizungumza na Baada ya semina hiyo Mratibu wa mashindano hayo Elia Kitomo amewataka Viongozi wa timu shiriki kusoma kanuni ambazo walikabidhiwa na kamati yake ili waweze kuzielewa na kuzifuata

Naye Diwani wa Kata ya Luhota amesema kuwa Ni muda muafaka kwa Viongozi wa vilabu hivyo kusimamia vyema nafasi zao katika mashindano hayo na kujiepusha na dhana ya kuingilia Majukumu ya Benchi la Ufundi.

Awali Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalenga kupitia katibu wake ilikabidhi mipira kwa vilabu ambavyo havukupewa Vifaa hivyo ili waweze kufanya mazoezi kijiandaa na ligi hiyo iliyopangwa kuanza Rasmi tarehe 26/8/2023 na zitachezwa kwa mfumo wa mtoano kuanzia ngazi ya Tarafa

Kwa mujibu wa Mdhamini wa Mashindano hayo Jackson Kiswaga, Bingwa atapata shilingi milioni Moja na Laki mbili na safari ya kwenda Zanzibar kucheza mechi siku 3, mshindi wa pili atapata shilingi Laki nane na mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi Laki sita.