Nuru FM

Heaven Safari and Tour’s, Kitomo hardware wamwaga vifaa Nzihi cup 2023

11 June 2023, 6:21 pm

Baadhi ya viongozi wa timu shiriki michuano ya Nzihi Cup 2023 wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupewa vifaa vya michezo. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Kampuni ya Heaven Safaris and Tour’s na Kitomo Hardware wamegawa vifaa vya michezo kwa timu shiriki kwenye michuano ya Nzihi Cup 2023 yatakayoanza kutimua vumbi Juni 17 mwaka huu huko kata ya Nzihi.

Vifaa vilivyogawiwa kwa viongozi wa vilabu hivyo ni jezi seti moja na mpira mmoja ambapo timu zilizopewa vifaa ni Nzihi FC, Kidamali FC, Kipera FC, Nyamihuu FC, Ibogo FC, Ilalasimba FC, Magubike FC, Mlambalasi FC na Mkombe FC.

Mkurugenzi wa makampuni ya Heaven Safari and Tour’s na Kitomo Hardware Elia Kitomo akizungumzia kuhusu udhamini wake kwenye ligi ya Nzihi Cup. Picha na Hafidh Ally

Akizungumza wakati wa semina elekezi kwa viongozi wa kata ya Nzihi, viongozi wa vilabu shiriki na manahodha wa vilabu hivyo, mdhamini wa mashindano hayo ambaye ni mkurugenzi wa makampuni hayo Elia Kitomo amesema kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha vijana wa kata hiyo wanaonesha vipaji vyao na kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza sekta ya michezo.

Diwani wa kata ya Nzihi Steve Mhapa akizungumzia kuhusu michuano ya Nzihi Cup 2023. Picha na Hafidh Ally

“Mimi ni mkazi wa Nzihi hivyo nimeona ni vyema nikarudi huku na kuwakumbuka vijana wa kata hii kwa kudhamini michuano hii, na kukuza sekta ya utalii, kwani kupitia kampuni zangu za utalii na ujenzi ninaweza kuwaonesha fursa za kiuchumi vijana wenzangu kwenye mashindano haya” Amesema Kitomo.

Kitomo amewataka vijana watakaoshiriki michuano hiyo kuwa na nidhamu ikiwemo kufuata kanuni na sheria za mashindano hayo ili wapatikane mabingwa ambao wataiwakilisha vyema kata ya Nzihi.

Naye diwani wa kata ya Nzihi Mh. Steve Mhapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo amesema kuwa baada ya kupata maombi kuhusu uwepo wa ligi ya Nzihi kutoka kwa vijana wa kata yake, aliamua kuwasiliana na mdau wa michezo ambaye ni mkurugenzi wa makampuni ya utalii Heaven Safari and Tour’s na Kampuni ya ujenzi ya Kitomo Hardware , kuhakikisha wanafanya mashindano hayo ili kuibua vipaji vyao.

Aidha Mhapa amesema kuwa bingwa wa michuano hiyo atapata jezi seti moja na shilingi 400,000/= huku mshindi wa pili akipata jezi seti moja na shilingi 250,000/= wakati mshindi wa tatu akipata jezi seti moja na shilingi 150,000/= huku timu zilizoshika nafasi ya nne mpaka ya tisa wakipata mpira mmoja kama pongezi kwa kushiriki.

Amesema kuwa timu mbili zitakazoingia fainali ya michuano hiyo zitaandaliwa mashindano mengine kutoka kata za jirani na kugombea zawadi ambazo zitatangazwa hapo baadaye.

Kwa upande wake Teonest Mbembe ambaye ni nahodha wa Nyamihuu FC na Maneno Fungo Kiongozi wa timu ya Kidamali FC wamemshukuru diwani wao na mdau Elia Kitomo kwa kuwaletea mashindano hayo yatakayowaepusha vijana na makundi hatarishi huku wakiahidi kufanya vizuri na kuwa mabingwa.

Katika semina hiyo iliyoendeshwa na mwamuzi mkongwe Rashid Zongo, kumefanyika zoezi la upangaji wa makundi ambapo kundi A linaundwa na timu za Magubike FC, Kipera FC, Nyamihuu FC, Ilalasimba FC na Mkombe FC, huku Kundi B likiundwa na Timu za Kidamali FC, Nzihi FC, Ibogo FC na Mlambalasi FC.