Nuru FM

Watumishi Mafinga Mji watakiwa kusoma mapato na matumizi

21 June 2023, 8:14 pm

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu Ayoub Kambi Akitoa maagizo kwa watumishi. Picha na Sima Bingileki

Na Sima Bingileki

Watumishi katika Halmashauri ya Mji mafinga Mkoani Iringa wametakiwa kuweka wazi na kuwasomea wananchi mapokezi ya fedha za miradi ya maendeleo kwenye mikutano ya Kata na mbao za matangazo kwani wananchi wanahaki ya kujua mapato na matumizi.

Akizungumza kwenye ziara ya Mkurugenzi ya Kusikiliza changamoto za watumishi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu, Ayoub Kambi amesema kuwa Katika Utumishi kuna Haki na Wajibu, hivyo kila mtumishi ahakikishe anatimiza wajibu wake anapodai Haki.

“ Nimepokea changamoto zenu na nitazufanyia kazi na ndo mana nimekuja na wataalamu wangu ili lile linaloweza kutatulika liishe na Yale yanayohitaji ufuatiliaji nayachukua kwa Utekelezaji mkifanya kazi kwa uwazi hakutakuwa na malalamiko Kwa Serikali.

Amesema malalamiko ya wananchi ngazi ya kata yatatuliwe na wananchi Wasikilizwe kwa kutumia lugha mzuri.

Aidha ameagiza Wataalamu Makao Makuu kufanya ziara na kutoa ufafanuzi kuhusu Masuala ya haki za watumishi na sera mbalimbali ili kuwajengea uelewa watumishi ngazi ya Kata.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watumishi wote Kata ya Bumilayinga na Kata ya Isalavanu wakiongozwa na Kaimu Mtendaji wa Kata ya Bumilayinga ndugu,Nikanileka Chaula, Mtendaji Kata ya Isalavanu Calvina Msovela, Wataalamu kutoka Makao Makuu Idara ya Utawala, Elimu Msingi na Sekondari .

Ziara ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu Ayoub Kambi Ni ziara ya kimkakati ambayo imeanza tarehe 21/6/2023 mpaka tarehe 6/7/2023.