Nuru FM

Kakakuona aonekana Iringa Atabiri

15 July 2023, 11:35 am

Kijana Asajile Mwajala aliyemshika Kakakuona akimkabidhi kwa Idara ya Wanyamapori. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Mnyama aina ya Kakakuona aliyemtabiria Mkulima Mkazi wa Kijiji cha Ihemi kupata mafanikio kupitia zao la Parachichi amekabidhiwa katika idara ya Wanyamapori Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi Mnyama hiyo ambaye alimuokota akiwa shambani kwake, Asajile Mwanjala amesema kuwa Mnyama huyo alimuona shambani kwake wakati akimwagilia mazao yake ya parachichi ndipo akaamua kutoa taarifa Polisi.

Mnyama aina ya Kakakuona amekuwa akitumiwa kiimani na baadhi ya jamii ikiwemo kuwatabiria mambo yao alionekana katika shamba la Asajile na ndipo akachukua jukumu la kumchukua na kumpeleka nyumbani kwake.

“Nilipofanikiwa kumkamata Kakakuona huyo ambaye ni mara ya pili kumuona baada ya awali kumwona na kumkamata kisha akanitoroka lakini safari hii nilipomkamata niliamua kupiga simu polisi kuwajulisha kuhusu Mnyama huyo ndipo wao wakanishauri niwasiliane na Idara ya Maliasili na wanyamapori” Alisema Asajile.

Asajile amesema kuwa kitu anachokijua kuhusu Kakakuona ni kutabiri mambo ya watu ambapo na yeye aliamua kujitabiria kwa kumwekea Jani la Parachichi, fedha na jembe lakini Kakakuona huyo alifika katika jani la Parachichi na hivyo kuamini kuwa atapata mafanikio kupitia zao la Parachichi.

Kakakuona aliyeonekana Katika Kijiji Cha Ihemi Mkoani Iringa. Picha na Hafidh Ally

Amewashauri wananchi wenzake kutowadhuru wanyama watakaowaona katika makazi yao na badala yake watoe taarifa kwa idara ya Wanyampori ili waweze kurejeshwa katika makazi yao.

Stanley Castory ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihemi amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya uwepo wa Kakakuona huyo alifika eneo la tukio na kumpigia simu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambaye alifika na timu ya wataalamu kwa ajili ya kumchukua.

Kwa upande wake Afisa wa Wanyapori kutoka Wilaya ya Iringa Charles Mdendeme amekiri kuonekana kwa Kakakuona huyo huku akiwataka wananchi kutowadhuru wanyama hao pindi wnapowaona na kuwataka watoe taarifa katika idara zao ili warejeshwe katika hifadhi zao.
“kakakuona ni mnyama ambaye ana thamani kubwa kuliko Tembo na ndio maaana tunasisitiza wananchi wasiwadhuru kwa sababu ni nadra sana kuwaona na ndio maana tukikukuta naye unachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo cha miaka 30 na kuendelea”

Bashiri Mhoja Ni Mkuugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa amesema kuwa Kakakuona huyo atarejeshwa katika makazi yake halisi baada ya kukabidhiwa kwa Maafisa wa wanyamapori.

Aidha amesema kuwa baada ya kakakuona huyo kumtabiria kijana kupata mafanikio kupitia zao la Parachichi Ofisi yake imesisitiza wananchi wengine kuwa na mwamko wa kulima zao hilo kwa wingi ili waweze kuuza kwa wingi na kukuza uchumi.

“Kama jinsi kakakuona huyu alivyomtabiria kijana Asajile kuwa atapata mafanikio kupitia zao la parachichi na sisi tunasisitiza wananchi waendelee kulima kwa wingi zao hilo, Mimi binafisi ndio mara ya kwanza kumuona hivyo naweka mkazo katika imani hiyo” alisem Muhoja.

MWISHO