Nuru FM

Wanawake Iruwasa watoa msaada kwa wagonjwa

8 March 2024, 4:40 pm

Bi Sakila kutoka Iruwasa akikabidhi zawadi katika hospital ya Rufaa Iringa. Na Mwandishi wetu.

Mashuka yaliyokabidhiwa Hospitalini hapo yatawasaidia wagonjwa wanaolazwa.

Na Mwandishi wetu

Ikiwa Leo ni Siku ya Wanawake Duniani wanawake kutoka Idara ya Maji Safi na Mazingira Iringa (IRUWASA) wametembelea Hospitali ya Rufaa Ya Mkoa wa Iringa na kutoa mashuka 20 kwa ajili ya wagonjwa.

Akizungumza kiongozi wa kundi hilo Restituta Sakila amesema wameamua kutoa mashuka hayo kwa wagonjwa kwasababu Hospitali ni sehemu ambayo mtu yoyote anaweza kwenda kupata matibabu hivyo mashuka hayo yatawasaidia wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo.

Lakini pia ametoa wito kwa jamii kuwa na tabia ya kuwatembelea wagonjwa na kuwapatia msaada kwani Kuna ambao wanakosa huduma za Msingi kutokana na kukosa Ndugu wa karibu.

Kwa upande wa Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt.Alfred Mwakalebela amewashukuru wanawake hao kwa zawadi hiyo na kuwataka kila wakipata nafasi kuwatembelea wagonjwa siyo lazima iwe siku ya wanawake.

“Mnifikishie salam kwa Mkurugenzi wakati wowote mnakaribishwa kutoa chochote kwa wagonjwa hata msipokuwa na kitu mnakaribishwa kuona wagonjwa”amesema Mwakalebela