Nuru FM

Mafinga Mji kupambana na utapiamlo

28 February 2024, 9:32 am

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt Linda Salekwa akifuatilia Ripoti ya Lishe. Picha Mwandishi wetu.

Na Hafidh Ally

Halmashauri ya Mji Mafinga imeweka mkakati wa kupambana na Utapiamlo kwa kuhakikisha Chakula kinatolewa shuleni.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshima Dkt. Linda Salekwa kwenye kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata,Mitaa, Vijiji kwa kipindi cha Robo ya Pili Oktoba- Disemba 2023.

“Tuendelee kupambana na Utapiamlo katika Halmashauri yetu ya Mji Mafinga, tuhakikishe chakula mashuleni kinatolewa wakati wa mchana na kila shule iwe na bustani za mbogamboga”

Aidha amewapongeza Watendaji Kata zote 9 za Halmashauri ya Mji Mafinga na Maafisa Lishe kwa kuendelea kutekeleza Afua za Lishe kwa Uchangiaji wa Chakula mashuleni, kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa Lishe.

Akitoa taarifa ya hali ya Lishe, Afisa Lishe Halmashauri ya Mji Mafinga, Bi Josephine Nyaoga amesema kuwa Halmashauri kuanzia ngazi ya familia inafuatilia lishe za watoto, vyakula vya kupunguza udumavu na ulaji wa vyqkula bora na matumizi chumvi yenye madini joto ili kupunguza hali ya udumavu kwenye jamii na kufuatilia watoto wenye utapiamlo na kutoa elimu kuanzia ngazi ya mtaa mpaka wilaya.

Naye Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu Ayoub Kambi amesisitiza watendaji wa Kata zote tisa za Halmashauri ya Mji Mafinga kuzidi kutoa elimu kuhusu utapiamlo na kuhamasisha wazazi kuendelea kuchangia chakula cha mchana mashuleni.