Nuru FM

Wauzaji nishati ya gesi wahimizwa matumizi ya mizani

21 May 2022, 11:14 am

Wauzaji na wasambazaji wa nishati ya gesi wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na mizani ya kupimia kiwango stahiki cha gesi kama sheria inavyoagiza.

Wito huo umetolewa na Meneja wa mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na Maji (EWURA), Kanda ya kaskazini Mei 20, 2022 Mhandisi Lorivii Long’idu katika semina ya wadau wa gesi iliyofanyika jijini Arusha.

“Ni kosa kisheria kuuza gesi bila kuwa na mizani kwahiyo mnapaswa kuhakikisha mnakuwa na na mizani ili kuepuka hatua Kali za kisheria kwa wale watakaobainika kutokuwa nayo,” amefafanua Mhandisi Long’ido.

Amesema bado wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaouza mitungi ya gesi bila kupima kitu ambacho ni kinyume na sheria kwani uzito unatakiwa kuonekana kabla ya mtumiaji wa mwisho hajaanza kuitumia.

“Mtumiaji wa gesi unatakiwa kuhakikisha umeona muuzaji akiwa amepima na umejiridhisha kabisa kuwa ni kiwango stahiki na kama ni pungufu basi pia utaona”, ameelekeza Meneja Long’ido.

Aidha amefafanuwa kuwa endapo wauzaji wa mitungi ya gesi watafuata sheria malalamiko ya wananchi juu ya ujazo hafifu yataisha na kuwataka wafanyabiashara kuwa waaminifu katika kazi zao.

“Pale Moshi tumeshawafikisha mahakamani wafanyabiashara wawili baada ya msako niwaombe tu ninyi ka wapo wanaofanya hivyo waache la sivyo sheria itawaadhibu,” amesisitiza.

Semina hiyo ya wafanyabiashara wauzaji na wasambazaji wa gesi iliandaliwa ikiwa na lengo la kuwapa uelewa juu ya umuhimu wa matimizi ya mizani kwa ushirikiano wa EWURA kanda ya kaskazini na Kampuni moja ya uuzaji wa Gesi nchini.