RC Iringa awataka wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote
23 October 2026, 09:06

Kheri amewataka viongozi mbalimbali Iringa kusimamia utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kuonya kwamba hatafumbia macho kiongozi mzembe.
Na Chacha Robert
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakati na kupunguza changamoto za gharama za matibabu wanapougua.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote awamu ya pili uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa, Kheri amesema wananchi wanapaswa kujipanga mapema kwa ajili ya matibabu badala ya kusubiri kuugua ndipo waanze kutafuta fedha.
Amesema gharama ya kujiunga na mpango huo ni shilingi 150,000 kwa kaya yenye wanachama mmoja hadi sita, huku uanachama ukiwa wa miezi 12.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Iringa, Agnes Chaki, amesema awamu hiyo inalenga kusajili kaya 13,086 zenye jumla ya wanufaika 31,170.
Chaki amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya NHIF, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, halmashauri na wadau wengine ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Credianus Mgimba, amesisitiza umuhimu wa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma za afya, huku akihimiza utoaji wa huduma kwa wakati, kwa uwazi na bila ubaguzi.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo, akiwemo Maria Kihongole na Maimuna Ally kutoka Manispaa ya Iringa, wameishukuru Serikali kwa mpango huo, wakieleza kuwa utawasaidia kupata huduma za matibabu kwa urahisi na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwao na familia zao.
Uzinduzi wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa mujibu wa masharti ya mpango huo.
