Nuru FM

RC Kheri: “Vijana tumieni mitandao kwa maendeleo”

9 September 2026, 10:22

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Vijana wa JKT Mafinga. Picha na Hafidh Ally

Teknolojia imekuwa kwa kasi na mitandao ya kijamii imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa manufaa yao na ya jamii.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia ipasavyo mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujiletea maendeleo, kujenga jamii yenye maadili na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Amesema hayo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Vijana wa JKT kwa Mujibu wa Sheria, Operesheni Linda Amani pamoja na Kundi la Kujitolea la Operesheni Nishati Safi, iliyofanyika katika Kikosi cha 841 JKT Mafinga.

Mhe. Kheri amesema licha ya teknolojia na mitandao ya kijamii kuwa na manufaa makubwa, baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kuhamasisha vitendo visivyofaa katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, amewataka vijana hao kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kijamii na kuhakikisha wanaitumia kwa mambo yenye manufaa kwao, jamii na Taifa kwa ujumla.

Sauti ya Kheri

Akitoa taarifa mbele ya mgeni rasmi, mwakilishi wa wahitimu wa mafunzo hayo amesema mafunzo waliyopitia yamekuwa kama jando na unyago kwao, kwa kuwa yamewapatia maarifa na ujuzi mbalimbali utakaowasaidia katika maisha yao.

Amesema miongoni mwa maeneo waliyopatiwa mafunzo ni ujasiriamali, kujitegemea, uzalendo, nidhamu na uwajibikaji, ambayo yatawawezesha kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii.

Sauti ya Msoma Risala

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambaye pia ni Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amewataka vijana hao watakaporejea katika maeneo yao kuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzingatia nidhamu, uzalendo, maadili na uwajibikaji.

Sauti ya Mabena

Brigedia Jenerali Mabena amewataka vijana hao kutumia maarifa na ujuzi walioupata wakati wa mafunzo katika kujenga maisha yao, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Amesisitiza kuwa vijana hao wanapaswa kuwa nguvu chanya katika jamii kwa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo, huku wakizingatia uzalendo na maslahi ya Taifa kwa ujumla.